SHILINGI BILIONI 4.2 ZAHITAJIKA KUCHAPISHA VITAMBULISHO
Idara ya Uhamiaji imelitaka Bunge la Kitaifa kuidhinisha bajeti ya shilingi bilioni 4.2 zaidi kugharimia uchapishaji wa vitambulisho vya kitaifa.
Hii inafuatia hatua ya Rais William Ruto kufutilia mbali ada ya shilingi 300 kwa wanaoomba vitambulisho kwa mara ya kwanza na pia kusitisha ada nyingine ya shilingi 1,000 kwa wale waliopoteza vitambulisho hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Katibu wa Idara ya Uhamiaji na Huduma za Raia Dkt. Belio Kipsang amesema pesa hizo zitasaidia kugharimia takriban vitambulisho milioni 6 vinavyokadiriwa kuchapishwa katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.
Aidha, ameongeza kuwa bajeti hiyo mpya itagharimia vitambulisho milioni tatu vipya na vingine milioni 3 kwa waliovipoteza.
Imetayarishwa na Maurine Amwayi
English 









































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































