CITY WAPEWA LIVERPOOL, ARSENAL WAPATA MTEREMKO FA
Manchester City wataialika Liverpool kwenye awamu ya robo fainali ya kipute cha FA Cup nchini Uingereza, kulingana na droo iliyofanyika jana usiku.
Baada ya kuwashtua wengi na ushindi dhidi ya Sunderland, klabu ya Port Vale inayokabiliwa na hatari ya kushushwa daraja kutoka League One na ambayo ndiyo timu ya daraja la chini zaidi iliyosalia kwenye kinyang’anyiro hicho, imepewa Chelsea kwenye awamu hiyo.
Chelsea walilazimika kutoka chini mara mbili kabla ya kuandikisha usindi wa mabao 4-2 dhidi ya Wrexham waliokuwa na kadi nyekundu katika Raundi ya 5, na wamepewa mtihani mwingine dhidi ya klabu kutoka daraja la chini.
Vale wameingia robo fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1954.
Viongozi wa Premier League, Arsenal, baada ya kuwabandua Mansfield, watachuana na timu ya Southampton inayoshiriki ligi ya Championship, katika kile kinachoonekana kuwa mteremko kwao.
Southampton waliibandua Fulham katika raundi ya 5 wikendi iliyopita kufuzu awamu hiyo.
West Ham United walioibandua Brentford kupitia matuta ya penalti jana usiku, watakuwa mwenyeji wa Leeds, walioibandua Norwich kwa kichapo cha mabao 3-0.
Mechi za robo fainali ya FA zitachezwa wikendi ya tarehe 4 na tarehe 5 mwezi ujao.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 




























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































