MTIHANI BADO UPO

Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya linasema kuwa wachezaji wanane wa timu ya taifa ya wanawake ya U-17, Junior Starlets, watafanya mtihani wao wa KCSE wa 2024 kama ilivyoratibiwa.
Timu hiyo inatarajiwa kucheza Kombe la Dunia la FIFA U17 kuanzia tarehe 18 Oktoba hadi 3 Novemba, huku mitihani ya KCSE ikitarajiwa kuanza tarehe 4 Novemba.
Akijibu ombi la FKF kuhusu mitihani maalum ya KCSE kwa watahiniwa hao, Mkurugenzi Mtendaji wa KNEC David Njengere alisema baraza litawasiliana na wasimamizi wa vituo vya shule sita zilizoathiriwa ili kuhakikisha watahiniwa hao wanafanya mitihani yao ndani ya kipindi cha mtihani.
Hata hivyo alisema ni watahiniwa wawili tu kati ya wanane ndio watakaoathirika na watakosa mitihani ya Kifaransa na Sayansi Kimu iliyopangwa kuanza mapema tarehe 22 Oktoba.
Njengere amewataka watahiniwa hao kuendelea kujiandaa na mitihani hiyo wakati wakiendelea na mazoezi huku akiiomba Wizara ya Michezo kuhakikisha wanafunzi hao wanarudi katika shule zao mara baada ya kumaliza ushiriki wao ili kufanya mitihani hiyo.
Imetayarishwa na Nelson Andati