CITY WAONYESHWA VIMULIMULI VYA BLUES
Bao la Enzo Fernandez dakika za mwisho ziliipa Chelsea pointi 1 muhimu kwenye sare ya bao 1 na Manchester City na kudidimiza matumaini ya City kushindana na Arsenal katika uwandaji wa taji la ligi kuu ya soka nchini Uingereza EPL.
Kiungo wa Uholanzi Tijjan Reijnders aliwaweka City kifua mbele kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika na licha ya vijana hao wa Pep Guardiola kubuni nafasi nyingi, walishindwa kumalizia kabla ya kupewa Monday Blues the Blues wasio na mkufunzi rasmi baada ya Enzo Maresca kuondoka mwishoni mwa wiki jana.
Chelsea ambao wameshinda mara moja pekee katika mechi 8 zilizopita za ligi, walikuwa chini ya kocha wa wachezaji walio chini ya miaka 21 Callum McFarlane.
Sare ya pili mfululizo kwa City inawaacha pointi 6 nyuma ya Arsenal, na pointi sawa na Aston Villa.
Kwenye matokeo mengine, Liverpool walipoteza pointi 2 muhimu baada ya Fulham kusawazisha katika dakika za mwisho, na kusababisha sare ya mabao 2, ambayo pia ni sare ya pili mfululizo kwa vijana hao wa Arne Slot.
Wakati uo huo, Manchester United walilazimisha sare ya bao 1 dhidi ya Leeds United kupitia kwa Matheus Cunha, msururu wa matokeo duni ukiendelea.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































