KOECH ATETEA UAMUZI WA TANZANIA KUMZUIA KARUA

Mbunge wa Belgut, Nelson Koech, ametetea hatua ya Tanzania kumzuia Martha Karua kuingia nchini humo, akisema kila taifa lina haki ya kudhibiti mipaka yake licha ya ujumuishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Koech, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Ulinzi, Ujasusi na Mahusiano ya Kigeni, amekiri kuwa tukio hilo ni la kusikitisha lakini akasisitiza kuwa Tanzania ina mamlaka kamili ya kudhibiti mipaka yake kama taifa huru.
Koech ameyasema haya kwenye mahojiano na runinga moja nchini akiongeza kuwa licha ya juhudi za ujumuishaji wa kanda zinazowapa raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uhuru wa kuvuka mipaka, kila nchi bado ina haki ya kuamua nani anaweza kuingia katika ardhi yake.
Imetayarishwa na Janice Marete