#Football #Sports

LIVERPOOL WAWAWEKA LOS BLANCOS GIZANI

Miamba wa soka nchini Uingereza Liverpool walirejelea ubora wao na kuwafundisha Los Blancos wa Real Madrid namna ya kucheza soka na kupata ushindi muhimu katika mtanange wa klabu bingwa barani Ulaya ugani Anfield jana usiku.

Ushindi wa bao 1-0 ukijiri baada ya vijana hao wa Arne Slot kutamatisha msururu wa kupoteza mechi 6 kati ya 7 Jumamosi dhidi ya Aston Villa, ulisisitiza mwamko mpya kwa mabingwa hao wa Uingereza.

Bao la pekee la mchezo lilitiwa wavuni na raia wa Argentina Alexis Mac Allister, baada ya wimbi la mashambulizi ambalo laiti isingalikuwa kwa kipa Thibaut Courtois wa Real Madrid, basi weupe hao wa Barnebeu wangebebeshwa shehena ya magoli.

Courtois aliokoa mashambulizi manne kutoka kwa Dominik Szoboszlai pekee, na kichwa cha Virgil van Dijk, kabla ya kulemewa na kichwa cha Mac Allister kutokana na ikabu ya Szoboszlai.

Ni mechi ambayo pia ilishudia kurejea kwa kijana aliyezaliwa na kulelewa Liverpool Trent Alexander-Arnold, ambaye makaribisho ya pekee yalikuwa ni kuzomewa na mashabiki wa Liverpool alipoingia kama nguvu mpya, huku Kyllian Mbappe na Jude Bellingham wakizimwa kabisa mchezoni.

Beki wa kulia wa Liverpool Conor Bradley aliyejaza pengo la Alexander-Arnold aliyehamia Madrid, alitekeleza jukumu lake kikamilifu la kuhakikisha kuwa nguli wa Brazil Vinicius Juniuor haonekani, hatua ambayo imeiondolea hofu Liverpool katika safu ya ulinzi.

Ushindi huo unawaweka Liverpool katika nafasi ya 6 kwenye jedwali la timu 32, wakiwa katika nafasi ya kufuzu kwa awamu ya timu 16 bila kuhitaji kushiriki mwondoano.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

LIVERPOOL WAWAWEKA LOS BLANCOS GIZANI

Wabaya Bayern wamzima bingwa PSG

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *