KAYOLE STARLETS WASHINDA BANDARI QUEENS 0-1 MOMBASA

Kayole Starlets waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Bandari Queens katika mechi yenye ushindani mkali ya Ligi ya Kitaifa ya Wanawake iliyochezwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Serani, jana Jumapili.
Bao hilo pekee lilifungwa na Esther Ngugi katika kipindi cha pili, likikomesha mfululizo mzuri wa matokeo kwa Bandari Queens kwenye ligi.
Kocha wa Kayole, Mary Odhiambo, alionyesha furaha tele kwa alama tatu muhimu za ugenini, akisema timu yake inasonga hatua kwa hatua kurejea Ligi Kuu. Kwa upande wake, Janet Amuga wa Bandari alihuzunika, akisema timu yake iliunda nafasi bora lakini haikuwa makini katika kuzitumia.
Happy Nyadzua alikosa nafasi ya wazi katika dakika ya nane baada ya kuunganisha krosi ya Saumu Baya, lakini juhudi yake ilipita karibu na goli kwa tofauti ya inchi chache huku kipa akiwa ameshindwa kuokoa.
Bandari waliendelea kushambulia na walikaribia tena katika dakika ya 25, lakini Baya alishindwa kufunga kufuatia kona nzuri iliyochongwa na Florida Sidhani.
Winga wa Kayole, Nuru Hadima, alipiga shuti lao la kwanza lililolenga lango katika dakika ya 30, lakini shuti lake kutoka umbali wa yadi 20 lilizuiliwa na kipa wa Bandari, Belinda Akinyi.
Hata hivyo, Kayole Starlets walikuwa wa kwanza kufurahia, walipopata bao la kwanza dakika 15 baada ya kipindi cha pili kuanza, ambapo Ngugi alipiga shuti la yadi 30 lililomshinda Akinyi.
Imetayarishwa na Janice Marete