TUSKER FC ROHO JUU DISEMBA HII
Kocha mkuu wa klabu ya Tusker FC Charles Okere anaamini kuwa ushindi wa kikosi chake wa bao 1-0 dhidi ya Ulinzi Stars hasa mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba umekiweka kikosi hicho katika mkondo wa kumaliza katika nafasi bora kwenye awamu ya kwanza ya ligi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Tusker walionyesha mchezo mzuri dhidi ya wanajeshi, Dennis Oalo akifunga bao la pekee la mchezo katika dakika ya 32 na kuwapa alama zote 3 muhimu.
Okere amesema ushindi huo unaashiria mwanzo wa mazuri hasa katika mwezi huu wa sherehe, kikosi chake kikiwa kimeshinda mechi 2 mfululizo kufuatia ushindi wa awali wa bao 1-0 dhidi ya Mara Sugar.
Kwa sasa wanajiandaa kwa mchuano wa katikati ya wiki watakapomenyana na Sofapaka Alhamisi hii.
Tusker watalenga kulipiza kisasi cha kulimwa mabao 7-1 na Sofapaka mwishoni mwa msimu jana.
Katika matokeo ya hapo jana, Posta Rangers waliisambaratisha Nairobi United kwa kichapo cha mabao 2-0, nayo Mathare United wakirambishwa sukari chungu ya Mara Sugar kwa kibano cha goli 1-0.
Kwa sasa Police FC wamepanda kileleni kwa pointi 20, wakiwa katika nafasi ya kutetea taji lao baada ya kipindi cha kusuasua.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































