MSHUKIWA WA UJAMBAZI AKAMATWA ENEO LA MALAVA KAUNTI YA KAKAMEGA

Maafisa wa polisi kaunti ya Kakamega wamemkamata na kumuzuilia mshukiwa wa ujambazi Jackson Mwangi Wangechi, mwenye umri wa miaka 38, ambaye amepatikana na silaha baada ya polisi kutekeleza operesheni katika maficho yake matatu.
Baada ya kupokea habari za kijasusi, maafisa hao wa polisi wamemfumania mshukiwa huyo katika eneo moja la burudani katika mji wa Malava, kabla ya kuandamana naye hadi nyumbani kwake ambapo silaha hizo zimepatikana.
Silaha hizo zinajumuisha vifaa vya kuvunja, mavazi ya kijeshi, risasi za mipira, bastola mbili, shoka, rununu zinazoshukiwa kuwa za wizi, vifunguo na vifaa vya mawasiliano.
Kupitia mtandao wa X, idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI imesema maafisa hao wameandamana na mshukiwa huyo hadi katika maficho mengine mawili ambapo wamepata vifaa vingine kama vile panga, funguo za gari aina Mazda Demio.
Kwa sasa mshukiwa huyo anazuiliwa na polisi huku uchunguzi ukiendelea.
Imetayarishwa na Janice Marete