CAPE VERDE YAFUZU KOMBE LA DUNIA MBELE YA CAMEROON
Timu ya taifa ya Cape Verde imefuzu mashindano ya kombe la dunia kwa mara ya kwanza katika historia baada ya kumaliza kileleni mwa kundi D, alama 4 mbele ya miamba wa soka barani Afrika Cameroon kwa alama 23.
Blue Sharks walikamilisha kampeni yao jana usiku kwa kuwanyuga Eswatini magoli 3:0, mabao ya Dailon Livramento, Willy Semedo na Stopira yakihakikisha kuwa kisiwa hicho kinatamatisha kampeni yake bila kupoteza mechi au kufungwa bao nyumbani, ikishinda mechi 4 kati ya 5 ukiwemo ushindi wa bao 1:0 dhidi ya Cameroon.
Indomitable Lions wa Cameroon walimaliza kwa sare tasa nyumbani dhidi ya Angola, na hivyo kumaliza katika nafasi ya pili kwa alama 19, sasa wakisubiri kushiriki mwondoano ili kusaka tiketi ya kuelekea Marekani kwa kombe la dunia mwaka ujao.
Cape Verde walikuwa sehemu ya mtawala wao wa awali Ureno hadi mwaka wa 1974, na kujiunga na FIFA mwaka 1982, mwaka ambao pia walijiunga na CAF.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 










































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































