GAVANA SANG AWAFUTA WAFANYIKAZI 1,100 WALIOAJIRIWA KINYUME CHA SHERIA ZA KAUNTI YA NANDI

Zaidi ya wafanyikazi 1,100 wa serikali ya kaunti ya Nandi waliopata ajira kinyume cha sheria wamefutwa kazi.
Gavana wa kaunti hiyo Stephen Sang amesema bodi ya utumishi wa umma ya kaunti iko mbioni kubatilisha barua zote za ajira ambazo zilitolewa kinyume cha utaratibu.
Wafanyikazi walioathiriwa, ambao majina yao yaliingizwa katika orodha ya mishahara ya kaunti bila utaratibu, hawatapata mishahara kuanzia mwezi huu.
Hatua hiyo inafuatia ukaguzi wa rasilimali watu uliofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma, uliobaini kashfa kubwa ya mishahara.
Mamia ya wafanyikazi – wengi wao wakiwa wapambe na jamaa wa maafisa wakuu wa kaunti – walipewa barua za kuajiriwa kinyume cha sheria na majina yao kuingizwa kwenye orodha ya malipo.
Imetayrishwa na Janice Marete