MBAPPE KUREJEA KIKOSINI
Kylian Mbappe anaweza kucheza mechi yake ya kwanza kwa Real Madrid watakapomenyana na Atalanta kwenye Super Cup ya leo saa nne usiku Uwanja wa Taifa wa Warsaw, Poland , lakini kocha Carlo Ancelotti amekataa kusema kama atamuanzisha.
Mbappe, 25, alitua katika mji mkuu wa Uhispania wiki iliyopita kuanza mazoezi na timu hiyo baada ya kujiunga na Real kama mchezaji huru kwa mkataba wa miaka mitano mwezi Juni, na hivyo kuhitimisha sakata ya uhamisho iliyovuma kwa miaka mingi.
Kocha huyo wa Italia alisema hapo awali kufuatia moja ya mechi za kirafiki za hivi majuzi za Marekani kwamba ni wachezaji walioshinda Ligi ya Mabingwa ndiyo wanapaswa kucheza Super Cup.
Ancelotti, hata hivyo, hakuondoa uwezekano wa Mfaransa huyo kupewa nafasi.
Alipoulizwa kama Mbappe anaweza kupewa majukumu ya kupiga penalti, meneja huyo alisema kazi hiyo itatolewa tu kwa mchezaji ambaye ataanza mchezo.
Real, ambao wametwaa vikombe vitano vya Super Cup hadi sasa, wana nafasi ya kuwa vinara wa taji hilo mbele ya Barcelona na AC Milan, ambao pia wameshinda mara tano.
Pia wanaweza kuweka historia msimu huu ikiwa wataanza kampeni yao kwa ushindi leo usiku, kwani kutakuwa na mataji saba kuwaniwa kwa mara ya kwanza kutokana na kuletwa kwa Kombe jipya la Mabara la FIFA (FIFA Intercontinental Cup).
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 





























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































