NAIBOIS KUANZA UTETEZI DHIDI LA L15 FC
Mabingwa watetezi wa taji la FKF Kenya Cup, Nairobi United, wataanza kampeni ya kutetea taji hilo dhidi ya L15 FC, inayoshiriki ligi la FKF kiwango cha kaunti ya Kilifi katika raundi ya timu 64 inayojumuisha timu kutoka ligii kuu hadi zile za mashinani.
Naibois, jinsi wanavyofahamika, waliwabandua miamba wa soka nchini Gor Mahia kutwaa taji hilo mwishoni mwa msimu jana kwa kichapo cha mabao 2-1 kwenye fainali.
Wakati uo huo, bingwa wa kihistoria wa taji hilo AFC Leopards, watamenyana na BB Bread FC mtaani Kayole kwenye mechi ya ufunguzi wanapolenga kutamatisha ukame wa miaka 9 bila kombe hilo ambalo walishinda mara 10.
Gor Mahia wataanza kampeni yao ugenini dhidi ya Dero FC kaunti ya Siaya, nao Tusker FC wakianza uwindaji wa kombe hilo kwa mara ya 6 watakapovaana na Mwea United, huku mabingwa mara 2 Bandari FC wakikabiliana na bingwa wa Sakaja Super Cup Githurai All Stars.
Murang’a Seal waliotinga nusu fainali msimu jana, watachuana na Kahawa Pride FC, huku bingwa wa mwaka 2023 Kakamega Home Boyz wakifanya ziara fupi kuelekea Kisumu watakapomenyana na Amani Youth FC.
Bingwa wa mwaka 2024 na bingwa mtetezi wa ligi kuu ya Kenya, KPL, Police FC, watakuwa na kibarua dhidi ya Embakasi United, nao Mara Sugar waliofika semi fainali msimu jana wakilenga kuwarambisha sukari chungu Wisdom FC ya Kitale, miongoni mwa ratiba nyingine.
Toleo la mwaka huu linajumuisha timu 15 kutoka ligi kuu, na 3 kutoka National Super League.
Bingwa atapokea shilingi milioni 3, mbali na kupata tiketi ya kuiwakilisha Kenya katika mashindano ya mashirikisho yaani CAF Confederations Cup.
Raundi ya 64 itaanza wikendi ijayo.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 







































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































