#Football #Sports

KIZAAZAA CHA EPL, LIVERPOOL WAUMWA NA WOLVES

Ushindani mkali unatarajiwa leo usiku katika mechi za ligi kuu ya soka nchini Uingereza, EPL, jumla ya mechi 5 zitakaposakatwa.

Darubini itaelekezwa kwenye pambano kati ya Arsenal ugenini dhidi ya Brighton, na Manchester City nyumbani dhidi ya Nottingham Forest.

Arsenal wanaoongoza ligi wakiwa pointi 5 mbele ya City, watakuwa na fursa ya kufungua pengo la pointi 8 kileleni iwapo City watamezwa na Forest, nao wapate ushindi kwenye mechi yao.

Hata hivyo, matumaini yao ya kubeba ligi huenda yakazikwa, iwapo maombi ya City kwamba njia ya Arsenal iingie giza na utelezi yatajibiwa, nao wavune pointi 3 dhidi ya wageni wao.

Ushindi wa City na kichapo kwa Arsenal utamaanisha pengo la pointi litapunguzwa hadi pointi 2, City wakiwa na mechi nyingine mkononi.

Katika ligi ambayo haiishi mshangao, mabingwa watetezi Liverpool waliumwa na Wolves jana usiku kwa kichapo cha mabao 2-1 ugani Molineux jana usiku.

Wolves ambao tayari wanajiandaa kushuka daraja mwishoni mwa msimu wakiwa mkiani mwa jedwali, walipata ushindi dakika za lala salama kupitia bao la Andre Neto, baada ya Mohammed Salah kufuta bao la Rodrigo Gomez.

Kwenye mechi nyingine, Manchester United watavaana na Newcastle ugenini, Fulham dhidi ya West Ham nao Aston Villa wamenyane na Chelsea.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *