ZETECH YASHINDWA KUINGIA KWA FAINALI YA RAGA

Kocha mkuu wa Zetech Oaks Ramsfield Matekwa ameelezea masikitiko yake baada ya wachezaji wake kushindwa kutinga mchujo wa fainali ya Ubingwa ambayo ingewahakikishia nafasi ya kuingia ligi kuu ya raga msimu ujao.
Oaks walikuwa wakitafuta kufuzu kwa ligi kuu kwa mara ya kwanza lakini wakabwagwa 41-9 na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) RFC.
Matekwa anasema kipigo hicho kiliwatamausha vijana wake lakini wataimarisha mazoezi yao ili kuwa tayari kupigania kupanda daraja msimu ujao.
MMUST RFC walikuwa wamecheza daraja la pili kwa misimu miwili iliyopita na uzoefu wao wa kucheza ligi kuu hapo nyuma ulikuwa muhimu kuwasaidia kupandishwa ngazi tena, pamoja na Daystar Falcons huku Mwamba RFC na South Coast Pirates ya Pwani Kusini wakishushwa daraja kutoka ligi kuu.
Imetayarishwa na Nelson Andati