MVUA YAWAZIMA BANDARI NA LEOPARDS, WATOKA SARE TASA MBARAKI

Bandari na Leopards waligawana pointi katika sare ya 0-0 jana Jumapili katika Uwanja wa Mbaraki, Mombasa, katika mchezo ulioathiriwa sana na mvua iliyonyesha kwa muda mrefu.
Pande zote mbili zilianza mchezo kwa tahadhari kwenye uwanja uliojaa maji, hali iliyobana kasi na ubora wa mchezo.
Nafasi za kufunga zilikuwa chache katika kipindi cha kwanza, ambapo washambuliaji wa Bandari, Beja Nyamawi na Alfred Emoni, walizuia na ulinzi thabiti wa Leopards.
Kwa upande wa AFC, Victor Omune na Musa Oundo walikumbwa na changamoto kupata nafasi nzuri za kufunga, huku wakishindwa hata kufyatua mpira kuelekea langoni.
Baada ya mechi, kocha wa Bandari, Ken Odhiambo, alionekana kuwa na matumaini licha ya matokeo hayo huku Kocha wa AFC Leopards, Fred Ambani, akionyesha kuridhika na matokeo kutokana na hali ya mvua na uwanja ulivyokuwa mgumu.
Imetayarishwa na Janice Marete