RIPOTI YAONYA KENYA HUENDA IKALEMEWA NA DENI
Mdhibiti wa Bajeti wa serikali Margaret Nyakang’o ametoa onyo kali kuhusu deni la umma linalokua kwa kasi nchini, ambalo limefikia Shilingi trilioni 11.73 kufikia mwisho wa Juni mwaka huu.
Katika Ripoti ya hivi karibuni ya Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya Kitaifa kwa mwaka wa fedha 2024-25, Dk Nyakang’o amebainisha kuwa serikali imekengeuka kwa kiasi kikubwa katika sera yake ya ukopaji, huku ukopaji wa ndani ukipita mikopo ya nje.
Hadi Juni mwaka huu, deni la ndani lilifikia shilingi trilioni 6.33, sawa na asilimia 54 ya deni lote, wakati deni la nje lilikuwa Sh5.4 trilioni (asilimia 46).
Chini ya utawala wa Rais William Ruto aliyeingia madarakani Septemba 2022, deni la umma la Kenya limeongezeka kwa takribani shilingi trilioni 3.
Ripoti ya Mdhibiti inahusisha ongezeko hilo na ukopaji wa kiholela ili kufadhili shughuli za serikali na miradi ya maendeleo huku kukiwa na upungufu wa mapato.
Imetayarishwa na Maureen Amwayi
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































