SHABANA YAJIWEKA MIONGONI MWA WAWANIAJI KPL
Ushindi mwembamba wa bao 1-0 wa Shabana FC dhidi ya Mathare United uliwapandisha na kuwaweka alama sawa na AFC Leopards, na hivyo kuiweka timu hiyo katika nafasi ya kuwania taji la ligi kuu ya soka nchini, KPL.
Bao la pekee la mchezo lilipachikwa wavuni na nahodha George Onyango dakika za jioni, na kuwapa vijana hao pointi 3 muhimu ligi hiyo inapoelekea ukingoni.
Kwa sasa wana pointi 40 sawa na Leopards, zikiwa ni pointi 6 pekee nyuma ya viongozi Gor Mahia, ingawa Shabana wamecheza mechi 22 nao Ingwe mechi 20.
Katika matokeo mengine, mkufunzi mpya wa Tusker FC Julien Mette, aliandikisha ushindi wake wa kwanza, vijana wake walipoizaba Murang’a Seal bao 1-0.
Bandari FC na Nairobi United walitoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1.
Hii leo, AFC Leopards wana fursa ya kupunguza mwanya wa pointi kati yao na Gor Mahia, watakapovamia wanabenki wa KCB.
Bidco watalenga kuikaanga sukari ya Mara Sugar, Ulinzi nao wakiwa kwenye misheni ya kuimarisha ngome yao watakapokutana na Kakamega Homeboyz.
Bingwa mtetezi Police FC, atatoana kijasho na Sofapaka.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 

































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































