THUNDER WALENGA KUNGURUMA BAL ELITE 16
Klabu ya Nairobi City Thunder inaanza kampeni yake katika michuano ya BAL Elite 16 Kanda ya Mashariki leo, ikiwa na matumaini ya kurejea katika hatua ya juu zaidi ya mpira wa vikapu barani Afrika.
Thunder itashuka katika uga wa michezo ya ndani uwanjani Kasarani kuvaana na Namuwongo Blazers wa Uganda, ambao waliingia kwenye hatua hii baada ya kumaliza nafasi ya pili katika mchujo wa Kundi D wa Ligi ya Daraja la Mashariki. Mechi yao ya pili itakuwa dhidi ya Johannesburg Giants kutoka Afrika Kusini, waliotawala Kundi E.
Katika makundi mengine, timu ya Ferroviaro Da Beira ya Msumbiji kutoka Kundi B itakutana na Bravehearts kutoka Malawi, ambao wanarejea Kasarani wakiwa na matumaini ya kujivunia kiwango kizuri zaidi baada ya kufanya vibaya mwaka jana.
Thunder inapigania nafasi ya kupata tiketi ya BAL 2026, ikiwa na nia ya kuboresha matokeo ya msimu uliopita ambapo walifika hatua ya mwisho lakini wakashindwa kunyakua nafasi kwenye fainali zilizochezwa jijini Pretoria.
Nahodha wa Thunder, Tylor Ongwae, amesema kuwa kikosi kimejipanga vilivyo na kinadhamiria kufidia matokeo duni ya mwaka jana, huku akiwaomba mashabiki wa Kenya kujitokeza kwa wingi.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 

























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































