TUKO TAYARI KWA OLIMPIKI

Makamu wa rais wa chama cha riadha nchini Paul Mutwii anasema wanariadha wa chini ya umri wa miaka 20 walioshiriki Mashindano ya Dunia ya U-20 mwaka huu huko Lima, Peru watakuwa tayari kwa Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles mnamo 2028.
Vijana hao walirejea nchini mapema leo baada ya kuvuna medali saba; tatu za dhahabu, tatu za fedha na moja za shaba, huku Kenya ikimaliza nafasi ya tano kwa jumla nyuma ya USA, Ethiopia, China na Jamaica mtawalia.
Sarah Moraa, ambaye alitumia dakika 2 sekunde 00.36 kushinda dhahabu katika fainali ya mbio za mita 800 kwa wanawake, alihusisha ushujaa wake na bidii na pia msukumo kutoka kwa binamu yake na bingwa wa dunia Mary Moraa.
Edmund Serem, ambaye alijinyakulia dhahabu katika fainali ya mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji kwa wanaume, anaamini kuwa ndiye atakayeweza kurejesha ubabe wa Kenya katika mbio hizo baada ya maumivu ya hivi majuzi katika Michezo ya Olimpiki ya Paris.
Imetayarishwa na Nelson Andati