LEICESTER YAMFUTA KAZI MENEJA STEVE COOPER
Leicester ilimfuta kazi meneja Steve Cooper, huku timu hiyo ikiwa na alama mbili tu juu ya eneo la kushushwa daraja katika Ligi Kuu ya Uingereza.
Cooper, mwenye umri wa miaka 44, hakuwa chaguo maarufu alipoajiriwa kuchukua nafasi ya Enzo Maresca mwezi Juni kutokana na historia yake na wapinzani wa karibu, Nottingham Forest.
Aliweza kushinda mechi mbili pekee kati ya 12 alizosimamia katika Ligi Kuu, hali iliyowaweka Leicester hatarini kushuka daraja. Kilichomaliza subira kilikuwa kipigo cha 2-1 kutoka kwa Chelsea kwenye mchezo wa Maresca wa kurejea King Power.
Kocha wa kikosi cha kwanza, Ben Dawson, atachukua jukumu la muda wakati klabu hiyo inakamilisha kutafuta meneja mpya.
Cooper alianza kazi yake ya ukocha katika mfumo wa vijana wa timu za taifa za Uingereza kabla ya kuwa na kipindi cha miaka miwili katika Swansea.
Hata hivyo, alipata umaarufu akiwa Forest, alipoiongoza timu hiyo, mabingwa wa Ulaya mara mbili, kurejea Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 23.
Hata hivyo, mafanikio hayo hayakumpa heshima kwa baadhi ya mashabiki wa Leicester, ambao walimpigia kelele hata kabla ya mchezo wake wa kwanza dhidi ya Tottenham.
Ushindi dhidi ya Bournemouth na wapinzani wa kushuka daraja Southampton haukutosha kupunguza mvutano na mashabiki.
Mfululizo wa mechi tano bila ushindi, ikijumuisha kuondolewa kwenye Kombe la Ligi na Manchester United, hatimaye ulimgharimu kazi yake huku Leicester ikiwa nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi.
Cooper anakuwa meneja wa pili wa Ligi Kuu kufutwa kazi msimu huu baada ya Erik ten Hag kuachana na Manchester United.
Imetayarishwa na Janice Marete
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































