#Football #Sports

NYOTA WA AFRIKA WAONGEZEWA WIKI NA FIFA

Wachezaji Nyota wa bara Afrika kama vile Mohammed Sala wa Liverpool, Bryan Mbeumo wa Manchester United na Achraf Hakimi wa PSG watachezea klabu zao kwa wiki moja zaidi hadi 15 mwezi huu kabla ya kujiunga na timu zao za taifa katika mashindano ya mataifa bingwa barani Afrika AFCON.

Haya ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirikisho la soka ulimwenguni FIFA, ambayo ni afueni kwa klabu hizo zinazokabiliwa na hatari ya kuwapoteza wachezaji wao mahiri kutokana na kipute cha AFCON kitakachoanza tarehe 21 mwezi huu hadi tarehe 18 mwezi ujao.

Kwa mujibu wa FIFA, uamuzi huo uliafikiwa kufuatia mashauriano ya kina na washikadau ikiwemo CAF, uamuzi ambao tayari umewakera makocha wa timu za taifa zinazoshiriki AFCON, akiwemo Tom Saintfiet wa Mali, na mwenzake wa Comoros Stefano Cusin ambaye ametaja uamuzi huo wa dakika za mwisho kama wenye kuvuruga.

Klabu nyingine zitakazowakosa wachezaji muhimu ni Manchester City kupitia kwa fowadi Omar Marmoush wa Misri,na beki wa kushoto Rayan Ait-Nouri wa Algeria, huku United ikiratibiwa kuwakosa Mbeumo, wing’a Amad Diallo wa Ivory Coast na Noussair Mazraoui wa Morocco.

Wakati uo huo, viongozi wa ligi Arsenal, Chelsea na Leeds United hawataathirika.

Klabu nyingine ambazo AFCON haitaziathiri kutokana na kukosa wachezaji wanaoshiriki ni Real Madrid, Barcelona, AC Milan na Juventus.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *