LIVERPOOL WAONYESHA MWANGA
Mkwaju wa penalti wake Dominik Szoboszlai katika dakika ya 88 uliwapa mabingwa wa Uingereza Liverpool ushindi muhimu dhidi ya wenyeji Inter Milan ya Italia katika kipute cha ligi ya klabu bingwa barani Ulaya.
Gumzo kubwa katika maandalizi ya mechi hiyo lilizingira fowadi wa Misri Mo Salah kuachwa nyumbani na kocha Arne Slot, baada ya matamshi yake katika vyombo vya habari wikendi iliyopita kwamba Liverpool inalenga kumsulubisha kutokana na msururu wa matokeo duni.
Ushindi wa jana unawaweka Liverpool katika nafasi ya 8 bora, ambayo inawawezesha kufuzu moja kwa moja awamu ya mwondoano.
Nao Inter wanashuka hadi nafasi ya 5, zikiwa zimesalia mechi 2.
Katika matokeo mengine, Chelsea waliendeleza msururu wa matokeo duni baada ya kupepetwa magoli 2-1 na Atalanta, Bayern München wakitoka nyuma na kushinda 3-1 dhidi ya Sporting.
Barcelona waliandikisha ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt.
Tukio kubwa katika mechi hiyo ya Bayern ulikuwa urejeo wa Alphonso Davies, ambaye amekuwa nje kwa siku 262 kutokana na jeraha.
Mechi zaidi zimeratibiwa kuchezwa leo usiku, ambapo Manchester City watakuwa wageni wa Real Madrid, nao Arsenal wakilenga kuendeleza uongozi watakapomenyana na Club Brugge.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































