SHUJAA WATANGAZA USHUJAA WORLD RUGBY SVNS
Kikosi cha taifa cha raga cha wanaume Kenya Sevens maarufu kama Shujaa, kiliwika nyumbani kwa kuandikisha ushindi mara 4 kati ya 5 katika mkondo wa kwanza wa mashindano ya HSBC World Rugby Sevens Division 2, na kumaliza katika nafasi ya tatu kwa msimamo wa jumla katika uwanja wa Nyayo hapo jana.
Katika mashindano hayo yaliyopewa jina la Nairobi Sevens, Kenya ilipoteza mechi ya mwisho dhidi ya Amerika 21-5, Ujerumani ikiongoza kwa pointi 13 katika kipute kilichodumu wikendi nzima jijini Nairobi.
Eagles wa Amerika na Shujaa wa Kenya waliandikisha pointi 12 kila mmoja katika mtanange huo wenye ushindani mkali, timu hizo sawa na Ujerumani, zikipoteza mechi moja moja.
Kabla ya papurwa kucha na Eagles, Shujaa walionyesha ushujaa wao dhidi ya Uruguay, na kuwapa kichapo cha 17-7.
Hata hivyo, mambo yalienda segemnege kwa kikosi cha wanawake, Kenya Lionesses, waliomaliza katika nafasi ya 5 wakiandikisha ushindi mmoja pekee na kupteza mechi 4.
Argentina na Afrika Kusini walimaliza katika nafasi ya kwanza na pili kwa pointi 13 na 12 mtawalia, baada ya kuandikisha ushindi mara 4 na kupoteza mara 1.
Mkondo wa pili utaandaliwa nchini Uruguay tarehe 21 na 22 mwezi ujao, kabla ya Brazil kuandaa mkondo wa 3 wiki moja baadaye.
Timu zitakazomaliza katika nafasi 4 za kwanza baada ya mikondo 3 zitajiunga na timu 8 katika daraja la kwanza yaani World Rugby Sevens Divisioni 1 Series Championships, washindi wakitawazwa mabingwa huku timu 4 za mwisho zikishushwa daraja kurejea katika daraja la pili.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 







































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































