SIMBAS WAVUNA USHINDI MNONO KWENYE MICHUANO YA KOMBE LA AFRIKA
Kenya Simbas walianza safari yao ya Kombe la Afrika la Raga mwaka huu kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2027 kwa ushindi mnono wa 32-24 dhidi ya Uganda kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Kampala. Griffin Chao alianza kufunga dakika ya 20 kabla ya Barry Young kuongeza ‘tri’ ya pili, na kuifanya Kenya kuongoza 12-0. Uganda ilirudi mchezoni na kupunguza pengo hadi 12-7 wakati wa mapumziko.
Katika kipindi cha pili, Young aliendeleza uongozi wa Kenya na baadaye, Nahodha George Nyambua alitumia vyema makosa ya Uganda na John Kubu akamalizia. Kwa ‘tri’ nyengine ya Young, Simbas walisonga mbele 25-10. Hata hivyo, Uganda ilipambana dakika za lala salama baada ya kiki ya Adrian Kasito, na Wokorach kufanya mambo kuwa 29-24.
Huku presha ikiongezeka, Barry Young kwa mara nyingine tena aliiokoa Kenya kwa mkwaju wa mwisho ambao ulihitimisha ushindi huo. Simbas sasa wanatinga nusu fainali, ambapo watamenyana na Zimbabwe Jumapili, Julai 13, huku macho yao yakitazama kufika Australia 2027.
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 












































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































