TIMU YA GHANA KULAZIMIKA KUSHINDA MECHI ZOTE ZILIZOSALIA KUFUZU DIMBA LA AFCON

Timu ya Ghana iliyowahi kuwa bingwa wa kombe la AFCON sasa iko kwenye nafasi ngumu katika awamu ya muondoano baada ya kupiga sare ya kutofungana mabao na timu ya Sudan Kusini kwenye mechi iliyogaragazwa siku ya Alhamisi kule Accra Ghana.
Nafasi ya Ghana ya kufuzu sasa ni finyu baada ya kushushwa hadi nafasi ya tatu kwenye jedwali ya kufuzu dimba la AFCON.
Wana black stars sasa watalazimika kushinda mechi zao zilizosalia ikiwa wanataka kufufua matumaini yao ya kucheza AFCON. Kwa sasa Ghana wako katika nafasi ya tatu katika Kundi F, pointi nne nyuma ya Angola na mbili nyuma ya Sudan.
Angola watakuwa wenyeji wa Niger mjini Luanda siku ya Ijumaa na ushindi wao wa nyumbani utawasogeza kwa pointi saba mbele ya mabingwa mara nne wa Afrika Ghana kwenye mchujo.
Mataifa yatakayomaliza katika nafasi ya kwanza na ya pili zitafuzu dimba la AFCON zitakazofanyika Morocco. Iwapo Sudan itaifunga Ghana siku ya Jumanne Ghana, maarufu Black Stars itakuwa imetoweka.
Tangia watinge nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya 2017, Ghana imekuwa ikisuasua kwenye dimba la AFCON na hata kupoteza katika hatua ya 16 miaka ya 2019 na kisha kutolewa mara mbili baada ya hatua ya makundi.
Imetayarishwa na Ken Osoro