BARCELONA KUMENYANA NA REAL MADRID

Barcelona itamenyana na wapinzani wao Real Madrid katika fainali ya Copa del Rey baada ya kuwalaza Atletico Madrid 1-0 kwenye Uwanja wa Metropolitano na kukamilisha ushindi wa jumla wa 5-4.
Kufuatia msisimko wa mabao nane katika mkondo wa kwanza wa nusu fainali huko Barcelona, bao la Ferran Torres dakika ya 27 lilitosha kuipa timu hiyo ya Catalan ushindi katika mji mkuu wa Uhispania kutinga fainali huko Seville baadaye mwezi huu, jambo ambalo halijatokea kwa zaidi ya muongo mmoja.
Real na Barca wamekutana katika fainali ya Copa del Rey mara 18 huku Real wakiongoza kwa kushinda mara 11, ikiwa ni pamoja na ushindi wa 2-1 katika fainali ya 2014 huko Valencia.
Timu zote mbili bado ziko kwenye kinyang’anyiro cha kuwania mataji matatu msimu huu huku zikifuzu kwa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na kumenyana katika mbio zinazoonekana kuwa za farasi wawili kuwania taji la LaLiga.
Real itasafiri hadi London kumenyana na Arsenal katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wiki ijayo huku Barca wakiwakaribisha Borussia Dortmund. Watakutana katika fainali ya Copa del Rey mnamo Aprili 26 kwenye Uwanja wa La Cartuja.
Imetayarishwa na Nelson Andati