SAFARI YA GOR YAANZA KWA UBAYA
Gor Mahia walianza safari yao ya Kombe la Kagame kwa mkosi baada ya kufungwa 1-0 na Red Arrows ya Zambia katika mchezo wa Kundi B uliochezwa jana usiku katika Uwanja wa Chamazi Sports Complex, nchini Tanzania.
Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa kocha Leonardo Neiva kuinoa Gor Mahia, na aliamua kwenda na kikosi cha kwanza kilichojumuisha wachezaji wazoefu lakini kukawa na nafasi kwa mchezaji mpya aliyesajiliwa Samuel Kapen.
Wazambia hao walifunga bao hilo dakika ya 74 kupitia kwa James Kamanga aliyetokea benchi.
Matokeo hayo yanaifanya Gor Mahia kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi lao ikiwa na pointi sifuri. Al Hilal ya Sudan, ambao mapema jana waliifunga Telkom ya Djibouti 2-0, wanaongoza kundi hilo. Mchezo unaofuata wa Gor ni dhidi ya Telkom Jumapili usiku.
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































