UCHOVU ULICHANGIA BUNGOMA QUEENS KUSHINDWA

Nahodha wa Bungoma Queens Centrine Simiyu amesema kwamba uchovu ulichangia kichapo chao cha jana cha mabao 10-0 dhidi ya Ulinzi Starlets.
Simiyu amesema walichelewa katika safari yao kuelekea mjini Kisumu ilikoandaliwa mechi hiyo, ya ligi kuu soka nchini Kenya hivyo basi kuingia ugani katika hali ya uchovu.
Centrine sasa anawaomba wasimamizi wa klabu hiyo kuchangamka zaidi katika mipango yao hususan kwa mechi za mbali ili kuepuka aibu kama hizo.
Ilikuwa mechi ya kufunga msimu na Bungoma Queens walihitimisha ligi wakiwa nafasi ya 6 kwa alama 19, huku wenzao Ulinzi wakimaliza katika nafasi ya 3 kwa alama 41.
Imetayarishwa na Nelson Andati