NAIROBI UNITED WAINGIA AFRIKA

Mabingwa wa ligi ya NSL Nairobi United wamejikatia tiketi ya kushiriki mashindano ya kombe la mashirikisho ya bara Afrika yaani CAF Confederations, baada ya kutawazwa mabingwa wa kombe la FKF Cup hapo jana.
Naibois ambao wamekuwa na mazoea ya kuwaangusha mababe wa soka nchini, waliwacharaza Gor Mahia kibano cha mabao 2:1 kwenye fainali za kombe hilo katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex hapo jana, na kujihakikishia ubingwa wa mataji mawili msimu huu, likiwemo lile la NSL.
Nairobi United ambayo vile vile imepandishwa daraja kushiriki ligi kuu KPL msimu ujao, iliizima ndoto ya Gor Mahia kupata nafasi katika mashindano ya bara, mabao yake yakifungwa na Frank Ouya na Enock Machaka, huku bao la Gor likifungwa na Ben Stanley.
Aidha, Gor walipoteza nafasi ya kusawazisha mambo kunako dakika ya 86 baada ya Austin Odhiambo kuangushwa katika eneo la hatari ila Alpha Onyango akapoteza mkwaju wa penalti.
Miongoni mwa miamba wa soka walioangushwa na katika safari ya Nairobi United kuelekea fainali ni Tusker FC, Kakamega Homeboyz, Mara Sugar na wanabenki wa KCB FC.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa