Wabaya Bayern wamzima bingwa PSG
Pambano la kubaini timu bora barani Ulaya baina ya bingwa mtetezi wa klabu bingwa barani Ulaya PSG ya Ufaransa na miamba wa soka wa Ujerumani Bayern Munich liliishia kwa bingwa kudhalilishwa nyumbani na wachezaji 10 wa Bayern baada ya kugaragazwa mabao 2-1.
Kiungo wa zamani wa Liverpool Luiz Diaz alijitwika jukumu la kuwafungia mabingwa hao wa Ujerumani mabao hayo mawili, na kuendeleza rekodi ya ushindi kwa Bayern ambao sasa wanajivunia ushindi wa mechi 16 mfululizo katika mashindano yote msimu huu.
Kulikuwa na mchanganyiko wa matukio katika kipindi cha kwanza wakati mfungaji Diaz alitimuliwa uwanjani kwa kadi nyekundu, baada ya kumwangusha Achraf Hakimi.
Licha ya kusalia 10, Bayern wanaonolewa na nahodha wa zamani wa Manchester City Vincent Kompany walihimili mashambulizi ya wenyeji wao, licha ya Joao Nevez kufunga bao la kufuta machozi katika dakika ya 74, PSG wakionja kichapo cha kwanza msimu huu katika mashindano hayo.
Bayern kwa upande wao wanaongoza jedwali kwa pointi 12 baada ya mechi 4 za ufunguzi.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 












































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































