RAGA YA KUKATA NA SHOKA

Wapenzi wa raga wanahakikishiwa kushuhudia utamu uliokolezwa kwenye mkondo ujao wa Kabeberi 7s, mkondo wa nne wa Msururu wa Kitaifa wa Raga ya wachezaji 7 katika Uwanja wa RFUEA jijini Nairobi kati ya Ijumaa na Jumapili, na yatajumuisha kitengo cha kwanza na cha Pili kwa wanaume, na kitengo cha wanawake.
Kabras Sugar, ambao walishinda Dala 7s mjini Kisumu wikendi iliyopita, wako katika kundi A pamoja na Nakuru RFC, Strathmore Leos na Impala RFC.
Waandaji, Mwamba RFC, wako katika kundi D pamoja na KCB, MMUST, na MKU Thika.
Mwamba leo walipata ufadhili wa Ksh.4.25 milioni kutoka kwa kampuni kadhaa zikiwemo Kenya Breweries kupitia chapa yake maarufu ya Tusker na CIC Insurance.
Mwenyekiti wa Klabu ya Mwamba, Jason Braganza, alikiri wanapitia changamoto lakini ufadhili huu utawasaidia pakubwa.
Wakati huo huo, shindano la wanawake linarejea kwa mkondo wa pili wa Kabeberi 7s.
Timu za wanawake ni pamoja na Kenya Harlequins, Mwamba Ladies na Nakuru Ladies.
Imetayarishwa na Nelson Andati