#Football #Sports

INGWE YAWARARUA GLAMOUR BOYS

Klabu ya AFC Leopards ilitangaza hatari kwa viongozi wa ligi kuu ya soka nchini, KPL, kufuatia ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Shabana FC ugani Nyayo hapo jana.

Kwenye mechi iliyotarajiwa kuwa na ushindani, Ingwe walitoa kucha na kuwaparura Glamour Boys kuanzia dakika za ufunguzi za mchezo.

Samuel Semo aliwaweka Ingwe mbele katika dakika ya 17 kutokana na mpira wa ikabu, kabla ya Tyson Otieno kufunga la pili katika dakika za lala salama kwenye kipindi cha kwanza baada ya kuandaliwa krosi safi na Ronald Sichenje.

Baada ya Victor Omune kupoteza nafasi ya kuwaweka Ingwe kwenye usukani kipindi cha pili, Wycliffe Awiko aliifungia Shabana bao la kwanza, ambalo baadaye liliwafuta tu machozi.

Samuel Ssenyojo aliwarejeshea Ingwe uongozi wa mabao mawili, kabla ya mechi hiyo kusitishwa kwa muda kutokana na taharuki uwanjani kati ya wafuasi na walinda usalama.

Kayci Odhiambo alifunga bao la 4 katika dakika ya 70 kabla ya Ssenyojo kurejea tena na kuzima matumaini ya Shabana FC kurejea mchezoni.

Ushindi huo unapunguza pengo la uongozi kati ya Ingwe na Gor hadi pointi 6, baada ya viongozi hao Jumamosi kuchupa kileleni na uongozi wa pointi 9 kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya Mathare United.

Leo ni zamu ya Kakamega Homeboyz dhidi ya APS Bomet, huku Ulinzi Stars wakilenga kujiwekea ulinzi dhidi ya kukaangwa na Bidco United.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *