SIJUI LOLOTE ASEMA POSTECOGLOU

Mkufunzi wa Tottenham Ange Postecoglou anasema “hajui” kuhusu ripoti zinazomhusisha, na kazi ya ukufunzi wa timu ya taifa ya Uingereza.
Postecoglou, 58, alisisitiza kuwa anashughulikia jukumu lake kama kocha wa Spurs baada ya Gareth Southgate kujiuzulu siku ya Jumanne.
Southgate, ambaye aliteuliwa 2016 na alikuwa amebakiza miezi mitano kwenye mkataba wake na Uingereza, alijiuzulu chini ya saa 48 baada ya Uhispania kuwafunga Three Lions kwenye fainali ya Euro 2024.
Kocha wa zamani wa Celtic, Postecoglou alichukua mikoba ya Tottenham mwanzoni mwa msimu uliopita na kuwaongoza kumaliza katika nafasi ya tano kwenye Ligi ya Premia.
Licha ya kukosa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa, Muaustralia huyo, ambaye aliifundisha timu yake ya taifa kuanzia 2013-17, alisifiwa kwa mtindo wake wa soka la kushambulia.
Meneja wa Newcastle Eddie Howe ndiye anayeongoza kuwania nafasi ya meneja ajaye wa England, lakini mtendaji mkuu wa Magpies Darren Eales amesema watapinga mbinu zozote kutoka kwa Chama cha Soka.
England itamenyana na Jamhuri ya Ireland tarehe 7 Septemba katika Ligi ya Mataifa.
Imetayarishwa na Nelson Andati