WASHUKIWA WATATU WA WIZI WAKAMATWA

Maafisa wa upelelezi kutoka Kilimani wamewakamata washukiwa watatu kuhusiana na wizi wa hali ya juu uliotokea Westlands, Nairobi, mwezi mmoja uliopita.
Washukiwa hao ambao walipatikana wamejificha huko Kawangware, wanaaminika kuiba pesa taslimu na vitu vya thamani ya mamilioni kutoka kwa raia wa Sudan Kusini anayeishi kando ya Barabara ya Rahpta, Westlands jijini Nairobi.
Tukio hilo lililotokea Septemba 24, lilishuhudia mwenye nyumba akirejea na kukuta nyumba yake ikiwa imeharibika, mlinzi wake hayupo, na pesa taslimu dola 24,500 pamoja na vifaa vya kielektroniki kuibiwa.
Wizi huo uliripotiwa mara moja katika afisi za Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI huko Kilimani, na kusababisha uchunguzi wa haraka.
Kulingana na ripoti za polisi, uchunguzi wa kitaalamu umepelekea wapelelezi kwenye maficho ya washukiwa, ambapo aina mbalimbali za vitu vipya vilivyopatikana vinavyoaminika kuwa mapato ya wizi vimepatikana.
Imetayarishwa na Janice Marete