DROO YA CAF CONFEDERATIONS
Jumla ya klabu 16 zinasubiri kwa hamu kufahamu wapinzani wao katika awamu ya makundi ya mechi za mashirikisho bara Afrika yaani CAF Confederations Cup itakayoandaliwa tarehe 3 mwezi ujao nchini Afrika Kusini.
Timu hizo, ikiwemo mwakilishi wa pekee wa Kenya Nairobi United, zilifuzu awamu ya makundi baada ya mkondo wa pili kutamatika wikendi iliyopita, zikijumuisha miamba wa soka barani, mabingwa wa zamani Pamoja na machipukizi ambao wameonyesha ari ya kuandikisha historia.
Awamu hiyo ya makundi inawaleta Pamoja miamba kama vile Zamalek, Wydad, na USM Algiers, na chipukizi kama vile Nairobi United, Stellenbosch na Singida ambao wanawakilisha kizazi kijacho cha miamba wa Afrika.
Mataifa Matano ambayo ni Morocco, Afrika Kusini, Tanzania, Algeria na Misri yana wawakilishi 2 kila taifa, huku uhasama wa kimaeneo ukitarajiwa.
Timu hizo zitajumuishwa katika makundi 4 ya timu 4.
Droo ya klabu bingwa barani Afrika pia itafanyika siku hiyo, ikijumuisha timu 16.
Tayari timu 14 zimefuzu awamu hiyo ya makundi, zikisubiri mshindi kati ya bingwa mtetezi Pyramids dhidi ya Ethiopian Insurance, na RSB Berkane dhidi ya Al Ahly Tripoli.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 


























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































