LIONEL MESSI NJE!

Nahodha wa Argentina aliyejeruhiwa Lionel Messi ameachwa nje ya kikosi kilichotangazwa Jumatatu na FA ya Argentina kwa ajili ya mechi ya mwezi ujao ya kufuzu Kombe la Dunia kwa mechi za ukanda wa Amerika Kusini dhidi ya Chile na Colombia.
Messi mwenye umri wa miaka 37 hakujumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 28 kufuatia jeraha la kifundo cha mguu wakati wa fainali ya Copa America mwezi uliopita nchini Marekani.
Mchezaji huyo wa Inter Miami kwa sasa anaendelea kupata nafuu katika klabu yake.
Kipa wa River Plate Franco Armani pia aliachwa nje ya kikosi, pamoja na mshambuliaji Angel Di Maria, aliyetangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa baada ya michuano ya Copa America.
Kocha Lionel Scaloni aliwataja kiungo Ezequiel Fernandez na mshambuliaji Valentin Castellanos kwa mara ya kwanza, pamoja na wachezaji chipukizi wakiwemo Alejandro Garnacho, Valentin Carboni, Valentin Barco na Matias Soule.
Argentina inawakaribisha Chile katika uwanja wa Monumental mjini Buenos Aires Septemba 5 kabla ya kumenyana na Colombia siku tano baadaye mjini Barranquilla.
Imetayarishwa na Nelson Andati