SHIRIKISHO LA FKF LALAUMIWA KWA UTOVU WA USALAMA UWANJANI
Mashabiki wa kandanda nchini Kenya wamelaumu Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kwa kukosa kutekeleza hatua za usalama za mashabiki katika viwanja vyote vya michezo nchini, na usimamizi mbovu wa soka wa humu nchini.
Mashabiki hao, chini ya Shirikisho la Mashabiki wa Soka la Kenya, KEFOFA, wameshutumu shirikisho hilo kwa kuendeleza ukosefu wa usalama wakati wa mechi, uhujumu wa uchumi, na kushindwa kujiandaa vya kutosha kwa matukio makubwa kama vile AFCON 2025.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Nairobi, Rais wa KEFOFA Francis Liboyi ametaka kukamatwa kwa wadau wakuu wa soka akiwemo Rais wa FKF Nick Mwendwa kwa kuhatarisha maisha ya mashabiki.
Liboyi pia alidai kuwa FKF imetenga uwakilishi wa mashabiki kutoka kwa Katiba yake, hivyo basi kuzima sauti za wafuasi wa soka nchini kinyume cha sheria.
Imetayarishwa na Nelson Andati
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































