MBAPPE AMILIKI LIGUE 2

Nahodha wa Ufaransa Kylian Mbappe amechukua nafasi ya mwanahisa mkubwa wa klabu ya Ligue 2 ya Caen, kampuni ya Mbappe Interconnected Ventures ilitangaza katika taarifa yake leo.
Mchezaji mpya wa Real Madrid, ambaye alikaribia kusajiliwa na Caen alipokuwa mdogo, amepata asilimia 80 ya hisa kupitia Coalition Capital, taasisi ya uwekezaji ya Interconnected Ventures, kuchukua nafasi ya uwekezaji wa Marekani wa Oaktree kama mwanahisa mkubwa.
Hakuna takwimu iliyotolewa rasmi lakini ripoti za vyombo vya habari vya Ufaransa zinaweka ada ya ununuzi kati ya Ksh.2 bilioni na Ksh.2.7 bilioni.
Mshindi huyo wa Kombe la Dunia mwenye umri wa miaka 25, ambaye sasa anakuwa mmoja wa wamiliki wachanga zaidi wa klabu ya kulipwa, aliandamwa na Caen alipokuwa na umri wa miaka 13 tu, kabla ya kujiunga na Monaco na kisha Paris Saint-Germain.
Caen Ilianzishwa mnamo 1913, na ilimaliza nafasi ya tano kwenye ligi kuu mnamo 1992 na kufika fainali ya Kombe la Ligi mnamo 2005 lakini wamecheza katika daraja la pili la ufaransa tangu 2019.
Imetayarishwa na Nelson Andati