OMANYALA HATASHIRIKI FAINALI YA LIGI YA DIAMOND
Ferdinand Omanyala, ambaye ni mwanariadha mwenye kasi zaidi barani Afrika amethibitisha kwamba hatashiriki Fainali ya Ligi ya Diamond 2025 mjini Zurich, Uswizi kutokana na majeraha anayougua.
Nyota wa Kenya, ambaye ni bingwa wa Afrika mara mbili na mshindi wa medali ya dhahabu ya Michezo ya Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 100, ametangaza hayo kupitia mikondo yake rasmi ya mitandao ya kijamii.
Omanyala alifichua kuwa amekuwa akipambana na maumivu ya nyonga, misuli , na eneo la gluteal katika wiki chache zilizopita, jambo ambalo limetatiza maandalizi yake kwa tukio hilo la kifahari.
Amesema usumbufu huo umeathiri uwezo wake wa kufanya vyema, hivyo kumlazimu kujiondoa kwenye Fainali ya Diamond League iliyopangwa kufanyika Agosti 27-28.
Aidha amesema kuwa ana matumaini ya kupona kwa wakati ili kuiwakilisha Kenya kwenye Riadha za Dunia zinazopangwa Tokyo, Japan, kuanzia Septemba 13 hadi 21.
Fainali ya Ligi ya Diamond ni mojawapo ya hatua zenye ushindani mkubwa katika riadha ya kimataifa, na kukosekana kwa Omanyala kunaonekana kuwa pigo kubwa kwa mashabiki wanaotamani kumtazama katika mchuano wa mita 100 wanaume, unaoratibiwa Alhamisi, Agosti 28 saa 9:27 Alasiri kwa Saa za Afrika Mashariki.
Imetayarishwa na Nelson Andati.
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































