WAKENYA WATIA FORA NEW YORK, KIPCHOGE AMALIZA WA 17
Mkenya Benson Kipruto alikaza Kamba dakika za mwisho na kumweka nje mkenya mwenzake Alexander Mutiso na kuibuka mshindi wa mbio za New York City Marathon hapo jana katika kinyang’anyiro cha kihistoria.
Kipruto aliandikisha muda wa saa 2, dakika 8 na sekunde 9, sekunde 0.16 mbele ya Mutiso na kuongeza taji hilo juu ya mataji mengine aliyopata katika ubingwa wa mbio za Chichago, Boston na Tokyo.
Mutiso, ambaye ni bingwa wa mbio za London Marathon mwaka jana, alitoa ushindani mkali na kutishia kuibuka bingwa hapo jana kabla ya kuzidiwa maarifa na Kipruto sekunde za mwisho.
Na katika kinachotarajiwa kuwa kinyang’anyiro chake cha mwisho, nguli wa riadha Eliud Kipchoge alimaliza katika nafasi ya 17, akiandikisha muda wa saa 2, dakika 14 na sekunde 36.
Kwa upande wa akina dada, mkenya Hellen Obiri ambaye ni bingwa wa New York Marathon mwaka 2023, alionyesha ueledi wake sekunde za lala salama na kuibuka bingwa kwa muda wa saa 2, dakika 19 na sekunde 51, na kuvunja rekodi ya miaka 22 iliyowekwa na mkenya Margaret Okayo mnamo mwaka wa 2003.
Obiri alikabiliwa na ushindani kutoka kwa wakenya wenza Sharon Lokedi na bingwa mtetezi Sheila Chepkirui.
Nyota wa Uholanzi Sifan Hassan alimaliza katika nafasi ya 6.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 


























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































