#Football #Sports

VIHIGA QUEENS WAJIANDAA KUKABILI MADIRA SOCCER ASSASSINS

Mabingwa mara nne wa Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake ya FKF, Vihiga Queens, wamejipanga vyema kuelekea mechi yao dhidi ya Madira Soccer Assassins itakayochezwa Jumamosi katika Shule ya Upili ya Nyang’ori, kaunti ya Vihiga, ligi hiyo ikirejea baada ya mapumziko ya wiki mbili.

Mapumziko hayo yalitokana na kambi ya timu ya taifa ya wanawake Harambee Starlets kujiandaa kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) ambalo hapo awali lilipangwa kuanza Machi 17 nchini Morocco kabla ya kuahirishwa hadi katikati ya Julai.

Kikosi kinachofundishwa na Boniface Nyamunyamuh kimekuwa kikifanya maandalizi makali kikilenga kujikusanyia alama zote tatu ili kupanda hadi kileleni mwa msimamo wa ligi. Vihiga Queens wako nafasi ya pili kwa alama 30 baada ya kucheza mechi 15, alama moja nyuma ya vinara na mabingwa watetezi Kenya Police Bullets ambao wamecheza mechi 13.

Imetayarishwa na Cyrus Sifuna

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *