REAL WAONYESHWA UBAYA NA BAYERN, ARSENAL YAPONEA
Miamba wa soka nchini Ujerumani Bayern Munchen waliweka miadi ya semi fainali ya kombe la klabu bingwa bara Ulaya na mabingwa watetezi Paris St-Germain, baada ya kuibuka kileleni katika pambano na Real Madrid lililoshuhudia mabao 7 yakifungwa jana usiku.
Mabao 5 yalifungwa katika kipindi cha kwanza cha kutoana kijasho katika mkondo wa pili wa robo fainali, kabla ya makocha kubadilisha mifumo ya mchezo katika kipindi cha pili kilichoshuhudia kasi ya mchezo ikipungua.
Kiungo wa Uturuki Arda Guler, alifunga bao la kasi zaidi kwenye mashindano hayo msimu huu, akiwaweka wageni Real kifua mbele baada ya sekunde 35 pekee za mchezo kutokana na makosa ya mlinda lango nguli wa Bayern na Ujerumani Manuel Neuer.
Hata hivyo, Bayern walijibu haraka kupitia Aleksandar Pavlovic katika dakika ya 6, Hari Kane akiifungia Bayern la pili baada ya Guler kuifungia Real la pili, naye Kyllian Mbappe akihakikisha Real wanaongoza kabla ya mapumziko.
Licha ya mabingwa hao mara 15 kuongoza kuelekea mapumzikoni, mambo yalikuwa sare ya jumla ya mabao 4-4 kutokana na kichapo cha mabao 2-1 katika mkondo wa kwanza wiki jana.
Mechi hiyo ilichukua mwelekeo tofauti kwa faida ya Bayern dakika za mwisho.
Mshambulizi wa zamani wa Liverpool, Luiz Diaz, alifunga bao la 3 katika dakika ya 89, dakika chache baada ya nguvu mpya wa Real Eduardo Camavinga kuonyesha kadi nyekundu baada ya kupokea njano ya pili kwa kupoteza muda.
Msumari wa mwisho kwenye jeneza la Real ulitiwa na Michael Olise dakika za majeruhi, na kuwapa Bayern ushindi wa mabao 4-3 usiku huo, na jumla ya mabao 6-4.
Katika matokeo mengine, Arsenal walilazimika kulinda bao lao moja kwa zaidi ya dakika 90 na kupata tiketi ya kutinga semi fainali kwa mara ya pili mfululizo, ambako watachuana na Atletico Madrid.
Bao la pekee la Kai Havertz katika mkondo wa kwanza wiki jana jijini Lisbon dhidi ya Sporting CP lilitosha, baada ya mechi ya marudiano hapo jana kuishia kwenye sare ya kutofungana.
Leo usiku, mechi za mkondo wa mwisho wa robo fainali za UROPA League na Conference League zitasakatwa.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 






































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































