FIFA WORLD CUP: DR CONGO WAIZIMA JAMAICA, ITALIA NJE GYOKERES AKIBEBA SWEDEN
Timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, ilijikatia tiketi ya kufuzu mashindano ya kombe la dunia kwa mara ya kwanza tangu miaka 52 iliyopita, baada ya kuilaza Jamaica bao 1-0 katika fainali ya mechi za mchujo wa mabara, Intercontinental play-off.
Katika mechi iliyosakatwa katika uwanja wa Guadalajara nchini Mexico, kiungo wa Burnley Axel Tuanzebe, alijipata katika kijisanduku na kuuelekeza mpira wavuni kutokana na kona ya Brian Cipenga kunako dakika ya 100.
Awali, mabao mawili ya Cedric Bakambu wa DRC yalifutiliwa mbali kutokana na ofsaidi, na licha ya juhudi za Jamaica na DRC, mechi iliishia sare tasa katika dakika 90 za kawaida.
Mara ya mwisho kwa Leopards kushiriki kombe la dunia ulikuwa mwaka wa 1974 wakiitwa Zaire, ambako walipoteza mechi zote za makundi na kufungwa mabao 14 kwa jumla bila jibu, kikiwemo kichapo cha mabao 9-0 dhidi ya Yugoslavia.
Hata hivyo, hiki ni kikosi cha kizazi kipya, ambacho kitalenga kufuta aibu ya miaka 52 iliyopita kitaposhiriki kombe la dunia nchini Marekani, Mexico na Canada mwezi Juni mwaka huu.
Timu ya taifa ya Iraq pia ilifuzu kombe hilo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 40, kutokana na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Bolivia katika fainali nyingine.
Katika matokeo ya fainali bara Ulaya, bingwa mara 4 wa kombe la dunia Italia maarufu kama the Azzurri, wapo nje kwa mara ya tatu mfululizo.
Hii ni baada ya kupoteza kwa mabao 4-1 kupitia mikwaju ya penalti dhidi ya wenyeji wao Bosnia and Herzegovina.
Licha ya kuchukua uongozi kunako dakika ya 15 kupitia kwa Michael Kean, Haris Tabakovic alifuta bao hilo kunako dakika ya 79, baada ya Italia kusalia wachezaji 10 kutokana na kadi nyekundu kwa Alessandro Bastoni.
Italia imeingia katika historia kama bingwa wa zamani wa kwanza kabisa kuwahi kukosa fursa ya kushiriki kombe la dunia mara tatu mfulululizo, baada ya kukosa mashindano hayo nchini Urusi mwaka 2018, na Qatar mwaka wa 2022.
Kwingineko, bao la mshambulizi wa Arsenal Viktor Gyokeres katika dakika ya 88 liliwapa Sweden ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Poland, na tiketi ya kushiriki kombe la dunia.
Vijana wa Graham Potter ambao walikuwa na kipindi kigumu katika mechi za makundi na kukosa kupata ushindi katika mechi yoyote, walionyesha kuimarika katika mechi za mchujo, Gyokeres akichukua jukumu la kuibeba timu hiyo, baada ya kufunga hattrick kwenye mechi ya semi fainali wiki jana.
Uturuki pia ilifuzu baada ya kuilaza Kosovo bao 1-0, nayo Jamhuri ya Czech ikailaza Denmark mabao 3-1 kupitia mikwaju ya penalti baada ya sare ya mabao 2-2.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































