#Football #Sports

UCL: YAMAL AKARIRI LIPO TUMAINI DHIDI YA ATLETICO

Mshambulizi wa klabu ya Barcelona Lamine Yamal, amesisitiza kuwa yeye na wachezaji wenza watapigania nembo ya klabu hiyo katika pambano la leo la mkondo wa mwisho wa awamu ya robo fainali katika kombe la klabu bingwa bara Ulaya watakapomenyana na Atletico Madrid.

Barcelona wana mlima wa kukwea kutokana na kichapo cha mabao 2-0 nyumbani katika mkondo wa kwanza wiki jana, na watahitaji kuwashinda vijana wa Diego Simeone na zaidi ya mabao 3 ugenini ili kufuzu nusu fainali.

Takwimu zinaonyesha kuwa miamba hao wa soka wa Uhispania wameshindwa kubatilisha kichapo kwenye mechi 6 za mwisho barani Ulaya walizopoteza wakiwa nyumbani, na inasubiriwa kuona iwapo watapata ushindi wa kwanza leo usiku.

Yamal anatarajiwa kuwa nguzo katika kampeni ya kuimarisha nafasi zao za kufuzu nusu fainali, na ameonya kuwa Barcelona itajituma hadi dakika ya mwisho kwenye mtanange huo.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 18,  amekuwa kwenye fomu nzuri msimu huu kwa Barca, akifunga mabao 22 na kuchangia mengine 18 katika mechi 43 ambazo amecheza katika mashindano yote.

Katika dimba la klabu bingwa, Yamal anajivunia mabao 5 na asisti 4 katika mechi 9, na atahitaji kuonyesha usogora wake jijini Madrid kuwasaidia miamba hao kufuzu awamu ijayo.

Katika pambano jingine, Liverpool watawakaribisha mabingwa watetezi Paris St. Germain, PSG ugani Anfield.

PSG wanaongoza kwa mabao 2-0 kutokana na ushindi kwenye mkondo wa kwanza, na watakuwa mbioni kulinda uongozi wao na kuwatumbukiza wenyeji wao kikaangoni.

Mechi zote zitaanza saa nne kamili.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *