FKF CUP KUINGIA RAUNDI YA 16 IJUMAA
Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka nchini KPL, Police FC, na washindani wa taji hilo Tusker FC watakuwa na kibarua kigumu katika raundi ya 16 ya kombe la FKF Cup hapo kesho katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi.
Police FC watakabiliana na Daudi wa soka BB Bread waliowabandua AFC Leopards na Gor Mahia, nao Tusker wakimenyana na Kariobangi Sharks walio katika fomu ya aina yake.
BB Bread waliizima leopards kupitia mikwaju ya penalty kufuatia sare ya mabao 2-2 katika raundi ya 64, kabla ya kuwalaza K’Ogalo kwa kichapo cha bao 1-0 katika raundi ya 32.
Kocha mkuu wa klabu hiyo Ajastine Okoba, amesema kikosi chake kitadumisha mbinu yao ya mchezo.
Kwa upande wao, Police wamefuzu awamu hizo kwa ushindi mnono, mwanzo wakiibandua Embakasi United na kisha ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya TBM Health.
Makocha wakuu wa Police na Tusker FC, Nicholas Muyoti na Juliene Mette mtawalia, wameonya vikosi vyao dhidi ya kulaza damu dhidi ya wapinzani wao kwenye mechi hizo za mwondoano.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 











































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































