HSBC: SHUJAA, LIONESSES WAMALIZA JUKWAANI BRAZIL
Timu za taifa za raga za wachezaji 7 kila upande, Shujaa ya wanaume na Lionesses ya wanawake, zilimaliza kwa kishindo kwenye mkondo wa mwisho mashindano ya kwanza ya HSBC Division 2, zikijizolea nishani za fedha kwenye mashindano hayo yaliyokamilika jana jiji Sao Paulo, Brazil.
Shujaa, ambao wamejikatia tiketi ya kushiriki dimba la Sevens World Championship katika juhudi za kusaka kupandishwa daraja, walishinda mechi 4 kati ya 5, na kumaliza katika nafasi ya 2 na pointi 18, ikiwa ni mara ya tatu kumaliza katika nafasi hiyo baada ya Nairobi na Montevideo.
Shujaa walitamatisha mkondo wa Sao Paulo kwa ushindi mnono wa 24-14 dhidi ya Uruguay, baada ya kuinyuga Marekani 31-14 hapo jana.
Ushindi mwingine ulikuwa 38-7 dhidi ya Ujerumani, 40-0 dhidi ya Canada, baada ya kichapo chembamba cha 14-12 dhidi ya Ubelgiji.
Kwa jumla, Shujaa waliandikisha pointi 50 na kufuzu kipute cha Sevens World Championships, ambako watamenyana na timu 8 za kwanza kutoka Division 1.
Walifuzu pamoja na viongozi Marekani walio na pointi 52, Ujerumani na Uruguay waliomaliza katika nafasi za 3 na 4 mtawalia.
Wakati uo huo, vipusa wa Kenya, Lionesses, walisaka blanketi kukiwa kumekucha baada ya kupata ushindi katika mechi 4 na kupoteza moja pekee kwenye mkondo wa mwisho, tofauti na mikondo ya awali ambako walionyeshwa kivumbi.
Lionesses pia walimaliza wa pili, kutokana na ushindi dhidi ya Argentina, Afrika Kusini, Uhispania na Uchina, kichapo cha pekee kikijiri mikononi mwa wenyeji Brazil.
Hata hivyo, hawatafuzu kwenye kipute cha kusaka ubingwa baada ya kumaliza katika nafasi ya 5 kwa jumla, wakiwa na pointi 40.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































