MURANG’A SEAL YAMTIMUA KOCHA MONDAY
Klabu ya Murang’a Seal inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini, KPL, imemfuta kazi kocha wake Osborne Monday, ikisema uamuzi huo uliafikiwa kufuatia makubaliano ya pande zote mbili.
Kwenye taarifa rasmi, Seal pia ilithibitisha kumtimua naibu kocha mkuu Philip Wanjoya, na kumteua mchezaji wa zamani wa Harambee Stars Dennis Odhiambo kuwa kocha mkuu mshikilizi wanaposaka mkufunzi mwingine.
Odhiambo ambaye pia aliwahi kuichezea Seal, KCB na Sofapaka alipokuwa mchezaji, anatarajiwa kuinoa klabu hiyo hadi mwishoni mwa msimu, akisaidiwa na Marcus Abwao.
Mechi yao ya kwanza itakuwa nyumbani dhidi ya Nairobi United.
Kufutwa kazi kwa wawili hao kulitiwa muhuri na kichapo cha mabao 5-1 dhidi ya Mfalme FC ya FKF Division One Zone D, na kubanduliwa nje ya kombe la FKF Cup katika raundi ya 16 wikendi iliyopita.
Kabla ya kutimuliwa kwake, Monday alikuwa na kipindi kigumu, akikabiliwa na msururu wa mechi 4 bila ushindi.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 





















































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































