AFCON 2025: SENEGAL WAVULIWA TAJI, MOROCCO WAVIKWA
Timu ya taifa ya Morocco imetangazwa kuwa bingwa wa dimba la taifa bingwa barani Afrika, AFCON 2025, baada ya shirikisho la soka barani humu, CAF, kubatilisha matokeo ya mechi ya fainali ambapo Senegal walishinda kwa bao 1-0.
Kabla ya ushindi huo, wachezaji wa Senegal waliondoka uwanjani kwa dakika 17 baada ya Morocco kupewa mkwaju wa penalti, mkufunzi wa Senegal Pape Thiaw akihisi kuonewa baada ya mwamuzi Jean Jacques Ndala awali kufutilia mbali bao la Ismaila Sarr.
Baada ya wachezaji hao kurejea uwanjani, kiungo wa Real Madrid Brahim Diaz alipoteza mkwaju huo wa penalti, kabla ya Pape Gueye kuwafungia Senegal bao la ushindi.
Hata hivyo kwenye uamuzi wake, bodi ya rufaa katika shirikisho la CAF imebatlisha matokeo hayo, kwa misingi kwamba kuondoka uwanjani kwa wachezaji wa Senegal kuliashiria kususia mechi, na hivyo kuwapa Morocco ushindi wa kawaida wa mabao 3-0 kwa mujibu wa sheria za shirikisho hilo.
Kwa mujibu wa kipengee cha 82 cha mashindano ya AFCON, iwapo timu itaondoka uwanjani kabla ya mechi kutamatika bila idhini ya mwamuzi, basi timu hiyo itatatangazwa kushindwa na kubanduliwa nje ya mashindano.
Kwa sasa Morocco ndio mabingwa wapya wa AFCON, ikisubiriwa kuona iwapo wataandaa sherehe jinsi Senegal walivyofanya wakati wa kutawazwa mabingwa Januari mwaka huu.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































