KLABU ZA UINGEREZA ZADHALILISHWA UEFA
Timu ya Newcastle United ya Uingereza ilikalifishwa kwa kichapo cha mabao 7-2 na Barcelona ya Uhispania, na hivyo kubanduliwa nje ya mashindano ya klabu bingwa bara Ulaya.
Barcelona walitinga robo fainali kwa jumla ya mabao 8-3 kufuatia sare ya bao 1-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza, na watacheza na wenzao wa La Liga Atletico Madrid.
Raphinha na Robert Lewandowski walifunga mara 2 Barcelona waliowararua Newcastle bila huruma.
Katika mechi ya kufana kwenye kipindi cha ufunguzi, Anthony Elanga alifunga mara mbili na kufuta mabao ya Raphinha na Marc Bernal, na Lamine Yamal alipofunga penalti dakika za majeruhi kipindi cha kwanza, ukawa ndio mwanzo wa mwisho wa Newcastle.
Licha Atletico yake Diego Simeone kupoteza mabao 3-2 dhidi ya Tottenham, walifuzu kwa jumla ya mabao 7-5 kufuatia ushindi wa mabao 5-2 katika mkondo wa kwanza.
Kwenye matokeo mengine, Liverpool walionyesha mchezo wa aina yake, na kuwacharaza Galatasaray mabao 4-0, na kuweka miadi ya bingwa mtetezi PSG katika awamu ya robo fainali, ambayo itakuwa ni mara ya kwanza kwa kocha Arne Slot kufika awamu ra robo fainali ya mashindano hayo.
The Reds amabo walikuwa chini bao 1-0 kutokana na kichapo katika mkondo wa kwanza, walisawazisha kupitia Dominik Szobozlai, kabla ya mkwaju wa penalti mwishoni mwa kipindi cha kwanza wake Mohammed Salah kuokolewa na kipa Ugurcan Cakir.
Hata hivyo, Liverpool, ambao ni timu ya pekee na Arsenal za EPL ambazo zimesalia kwenye mashindano hayo, walijikusanya kipindi cha pili na kupata mabao kupitia kwa Hugo Ekitike, Rayan Gravenberch na Salah.
Bao la Salah lilimfanya kuwa Mwafrika wa kwanza kufikisha mabao 50 katika mashindano ya klabu bingwa bara Ulaya.
Bayern Munich walioandikisha ushindi wa jumla ya mabao 10-2 dhidi ya Atalanta, watamenyana na mabingwa wa kihistoria mara 15 Real Madrid waliowabandua Manchester City.
Arsenal watachuana na Sporting CP ya Ureno.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































